Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kufuatia kutokea kwa shambulio la silaha dhidi ya hafla ya kidini ya Wayahudi katika mji wa Sydney, Australia, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Abulqasim Razavi, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa mji wa Melbourne, huku akionesha masikitiko makubwa kuhusu tukio hili chungu, alilaani vikali shambulio hilo na kutaja aina yoyote ya ugaidi na vurugu dhidi ya raia wasio na hatia kuwa ni kitendo kilichokataliwa na kisichokubalika.
Akiweka msisitizo kwamba; kuwalenga watu wasio na hatia kunapingana na mafundisho ya Kiislamu, maadili ya kibinadamu na misingi ya kimaadili ya kimataifa, alionya kuwa vitendo kama hivyo vya kikatili husababisha tu kuenea kwa chuki, ukosefu wa usalama na kuyumba kwa uthabiti wa jamii.
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Melbourne, katika hitimisho, aliitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua msimamo wa pamoja na thabiti, kusimama dhidi ya aina zote za ugaidi na vurugu, na kuchukua hatua madhubuti, pamoja na kuweka mazingira ya kufikiwa kwa amani, usalama na kuishi kwa maelewano duniani.
Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ilitoa tamko rasmi kulaani shambulio la silaha dhidi ya hafla ya Wayahudi huko Sydney, na kusisitiza kwamba aina yoyote ya ugaidi na kuwalenga raia wasio na hatia ni kitendo kilichokataliwa na kisicho na uhalali wowote, na ikataka kuchukuliwa hatua kali dhidi ya aina zote za ugaidi.
Ismail Baqaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), pamoja na kulaani vikali tukio hilo, alisisitiza kwamba mauaji ya watu na vitendo vya kigaidi wakati wowote na mahali popote ni mambo yaliyokataliwa kabisa na yasiyokubalika, na kwamba hakuna uhalali wowote wa vitendo kama hivyo vya kikatili.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, shambulio hilo lilitokea katika eneo la pwani la Bondi huko Sydney, sambamba na kufanyika kwa hafla ya kidini ya Wayahudi kwa munasaba wa sikukuu ya Hanukkah. Ufyatulianaji risasi katika tukio hili ulisababisha hasara za maisha na mali, na idadi ya washiriki waliuawa au kujeruhiwa. Baadhi ya vyombo vya habari vya lugha ya Kiebrania na vya Australia vimeripoti kuwepo kwa vifo na kujeruhiwa kwa idadi kubwa ya watu.
Waziri Mkuu wa Jimbo la New South Wales, akirejelea dalili za awali, alielezea tukio hili kuwa ni shambulio linalowezekana la kigaidi, na akatangaza kwamba inaonekana kitendo hicho kilifanywa kwa kuwalenga jamii ya Wayahudi. Polisi wa Australia pia wamethibitisha kuanza kwa uchunguzi mpana kwa ajili ya kuwatambua na kuwakamata wahusika wanaodhaniwa, na wametangaza kwamba bado hakuna kauli ya mwisho iliyotolewa kuhusu sababu na maelezo kamili ya shambulio hilo.
Maoni yako