Alhamisi 4 Desemba 2025 - 12:45
Je, Hazrat Ummul-Banin (s.a.) alifariki kiasili au aliuawa shahidi?

Hawza/ Pamoja na kwamba vyanzo vya kale vimekaa kimya kuhusiana na namna ya kufariki kwa Hazrat Ummul-Banin (s.a.), ripoti za baadaye zimewawekea watafiti simulizi mbili tofauti: kundi moja linaamini kuwa kifo chake kilikuwa cha kiasili, na kundi jingine, kwa kuzingatia nafasi yake kubwa ya kufichua maovu baada ya tukio la Ashura, linaamini kuwa alipewa sumu na Bani Umayya na kuuawa kishahidi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, tarehe 13 Jamadi al-Thani ni kumbukumbu ya kufariki kwa Hazrat Ummul-Banin (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake), na kwa mnasaba huu tunachapisha makala kumhusu bibi huyu mtukufu na mwenye cheo cha juu.

Miaka kumi baada ya shahada ya Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w) na Hazrat Fatima Zahra (s.a.), kwa mujibu wa wasia wa Hazrat Fatima Zahra (s.a.) mwenyewe, Hazrat Amirul-Mu’minin Ali (a.s.) alianza kufikiria kuoa mke mwingine, kwa sababu aliona tukio la Karbala mbele ya macho yake.

Aqil, kaka yake, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na kauli yenye uzito katika elimu ya nasaba, kiasi kwamba katika Msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) walimwekea mkeka wa kusalia, na makabila ya Kiarabu hukusanyika kumzunguka ili kupata elimu ya nasaba. Alikuwa mwepesi sana katika kujibu maswali ya waliomuuliza.

Kwa sababu hiyo, Ali bin Abi Talib (a.s.), alipokusudia kuoa, alimwambia kaka yake Aqil, ambaye alikuwa mashuhuri katika elimu ya nasaba na ambaye akili yake ilikuwa hazina ya siri za koo mbalimbali za Waarabu:
“Chagua mwanamke kwa ajili yangu kutoka katika kizazi cha mashujaa wa Kiarabu ili nimuoe, naye anizalie mtoto shujaa na mpanda farasi.”

Aqil akamchagulia Ummul-Banin kutoka katika ukoo wa Bani Kilab, waliokuwa mashuhuri kwa ushujaa usio na mfano, naye akamwambia ndugu yake:
“Oa Ummul-Banin al-Kilabiyya, kwa sababu hakuna walio maarufu kwa ushujaa kuliko baba zake na ukoo wake.”

Aqil pia alitaja sifa nyingine bora za ukoo wa Bani Kilab, na Imam akalikubali chaguo hilo, kisha akamtuma Aqil kwenda kwa baba wa Ummul-Banin ili kupeleka posa.

Maarufu kwa ushujaa na adabu

Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, Hazrat Ummul-Banin alizaliwa mwaka wa tano wa Hijra ya Mtume mtukufu wa Uislamu, katika mji wa Madina, kusini mwa Makka, miongoni mwa kabila la Hawazin, ndani ya ukoo mashuhuri wa Kilab, katika nyumba ya Hizam bin Khalid.

Baba wa Ummul-Banin alikuwa Abu al-Majl Hizam bin Khalid wa kabila la Bani Kilab, na baadhi ya wanazuoni wa siku hizi wamemtaja mama yake kuwa ni Thumama binti Suhayl bin ‘Amir bin Malik.

Nasaba ya baba na mama wa Ummul-Banin ilirejea kwenye makabila mashuhuri miongoni mwa Waarabu. Bani Kilab walikuwa maarufu kwa nafasi muhimu walizokuwa nazo kabla ya Uislamu, pamoja na ushujaa na upiganaji. Familia ya Ummul-Banin (a.s.) ilikuwa kinara katika heshima, ushujaa, uanaume, ukarimu na ujasiri, naye Ummul-Banin alirithi sifa hizi adhimu kutoka kwa babu zake.

Kuposwa kwa Ummul-Banin na Amirul-Mu’minin (a.s.)

Kabla ya posa ya Amirul-Mu’minin, Hazrat Ummul-Banin anasimulia: “Kabla ya posa hiyo, usiku mmoja niliota nikiwa nimekaa katika bustani yenye miti mingi na kijani kibichi. Palikuwa na mito inayotiririka na matunda mengi. Mwezi na nyota vilikuwa vinaangaza, nami nikawa ninavitazama na kutafakari juu ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Nilikuwa nikifikiria kuhusu mbingu iliyoinuliwa bila nguzo, na mwanga wa mwezi na nyota… Nilizama katika fikra hizi ghafla mwezi ukashuka kutoka angani na kukaa mapajani mwangu, na nuru ikatoka iliyoangaza macho. Nikiwa katika mshangao, nyota nne nyingine zenye nuru zikashuka pia na kukaa mapajani mwangu.”

Baba wa Ummul-Banin alimpeleka kwa mtafsiri wa ndoto wa kabila lao, naye akasema: “Usimwambie mtu yeyote ndoto hii. Jua kuwa mtu mkubwa kutoka kwa Waarabu na Wasiokuwa Waarabu atakuja kumposa binti yako, na Mwenyezi Mungu atampa kutokana naye wana wanne.”

Aqil alipokuja kupeleka posa kwa Hizam bin Khalid, baba wa Ummul-Banin alikumbuka ndoto ya kweli ya binti yake na kusema: “Kwa hakika Mwenyezi Mungu ametimiza ndoto yako, ewe mwanangu! Basi furahia kheri ya dunia na Akhera.”

Kisha akamwambia mkewe Thumama: “Je, unamuona binti yetu Fatima anafaa kuwa mke wa Amirul-Mu’minin? Jua kuwa nyumba yake ni nyumba ya wahyi, utume, elimu, hekima, adabu na maadili. Ikiwa unamuona binti yako anastahili nyumba hiyo, basi tukubali muungano huu uliobarikiwa.”

Ummul-Banin badala ya Fatima

Imeandikwa katika historia kwamba Hazrat Ummul-Banin alipofika katika nyumba ya Hazrat Ali (a.s.), alimpendekeza amwite kwa kuniya yake “Ummul-Banin” badala ya jina lake halisi Fatima, ili Hasan na Husayn (a.s.) wasimkumbuke mama yao Hazrat Fatima Zahra (a.s.) wakisikia jina hilo, na hivyo huzuni ya zamani isifufuke moyoni mwao na uchungu wa kukosa mama usiwaumize.

Ummul-Banin alipata watoto wanne katika nyumba ya Imam Ali (a.s.): Abbas, Abdullah, Uthman na Ja‘far, na kiongozi wao alikuwa Hazrat Abbas (a.s.), aliyezaliwa tarehe 4 Sha‘ban mwaka 26 Hijria mjini Madina.

Kila mmoja wa vijana hawa wanne waliotunzwa katika madrasa ya Ummul-Banin (a.s.) kwanza waliathiriwa na sifa bora za baba yao mtukufu Ali (a.s.), na pili wakajifunza adabu na kujitolea kutoka kwa mama yao, kiasi kwamba kila mmoja wao peke yake alikuwa mfano wa ujasiri, heshima, uungwana, uanaume, maadili na ukamilifu wa kibinadamu.

Wakati wa shahada ya kiongozi wa wachamungu Hazrat Ali bin Abi Talib (a.s.), mtoto mkubwa wa Ummul-Banin, yaani Abbas bin Ali (a.s.), alikuwa na umri wa karibu miaka 14, na ndugu zake walikuwa wadogo zaidi.

Baada ya Ashura

Baada ya tukio la Ashura, bibi huyu aliungana na Zaynab Kubra (s.a.), na kupitia maombolezo alipinga serikali ya Yazid. Kila siku alimshika mkono mtoto wa Hazrat Abbas (a.s.) na kwenda katika makaburi ya Baqi‘, akichora makaburi manne na kulia kwa vilio, watu nao hukusanyika kumzunguka, kiasi kwamba hata mtu mgumu wa moyo kama Marwan bin Hakam naye alilia kwa kilio chake.

Ummul-Banin baada ya shahada ya wanawe, kila siku alikuwa anakwenda Baqi‘ na kuomboleza kwa mashairi ya huzuni kali kwa ajili ya wanawe mashahidi. Watu wa Madina waliisikiliza msiba na vilio vyake hadi kufikia kiwango kwamba hata Marwan bin Hakam – adui wa Ahlul-Bayt – alikuwa anakuja kusikiliza na kulia.

Kifo au Shahada ya Ummul-Banin

Katika vyanzo vya kwanza vya hadithi na historia, hakuna taarifa ya mwaka wala namna ya kufariki kwa Ummul-Banin. Baadhi ya wanahistoria wa baadaye, kwa kurejea baadhi ya vyanzo, wameandika kuwa alifariki tarehe 13 Jamadi al-Thani mwaka 64 Hijria, lakini namna ya kufariki kwake haijafafanuliwa kwa uhakika.

Katika kitabu “Kanz al-Matalib” kilichoandikwa mwaka 1321 Hijria na Allama Sayyid Muhammad Baqir Qarabaghi Hamadani, kwa kunukuu kutoka katika kitabu “Ikhtiyarat”, imelipotiwa katika hadithi kwamba:
“Siku ya 13 Jamadi al-Thani, ambayo iliangukia siku ya Ijumaa, nilimtembelea Imam Zaynul-‘Abidin (a.s.). Ghafla Fadhl bin Abbas (a.s.) akaingia akiwa analia na kusema: Bibi yangu Ummul-Banin amefariki dunia. Kwa Mwenyezi Mungu, tazameni jinsi zama hizi za udanganyifu zilivyoifanya familia ya Kisaa’ waomboleze mara mbili ndani ya mwezi mmoja.”

Wengine wameandika kwamba kwa ujumla, kilicho wazi ni kwamba kifo cha Ummul-Banin kilikuwa cha kiasili tu, na hakuna ushahidi wa sababu maalumu ya kifo chake.
Lakini wanahistoria wengine wanaamini kwamba kwa kuzingatia nafasi ya juu ya Ummul-Banin katika kufichua dhuluma za Bani Umayya na mashairi yake ya maombolezo ya Karbala yaliyokuwa yanawaamsha watu dhidi ya watawala dhalimu, maadui walimtilia sumu kupitia asali yenye sumu na kuuwawa kishahidi.

Mwanahistoria mashuhuri Haj Sheikh Ali Falsafi katika kitabu Wanawake Wenye Kipaji na Abdul-‘Azim Bahrani katika kitabu Ummul-Banin wameandika kwamba; Bani Umayya walimtilia sumu mke wa Amirul-Mu’minin Ali (a.s.), yaani Ummul-Banin, na kumuua. Ummul-Banin amezikwa katika makaburi ya Baqi‘ karibu na Fatima binti Asad, mama wa Amirul-Mu’minin.

Vitabu Vilivyoandikwa Kuhusiana na yeye

“Nyota Inayong’aa ya Madina”, kitabu cha Ali Rabbani Khalkhali kuhusu Ummul-Banin, kilichochapishwa na Darul-Maktab al-Husayn. Kimetarjumiwa kwa Kiarabu na Sayyid Ali Jamal Ashraf kwa jina:
“Ummul-Banin al-Najm al-Sati‘ fi Madinat an-Nabi al-Amin”, kimechapishwa mwaka 2003 mjini Qum. “Ummul-Banin katika Kioo cha Mashairi”, kikiwa na utangulizi kuhusu maisha na karama zake, kimeandikwa na Muhammad Khurram Far, kilichapishwa Qum mwaka 1395 Shamsia. “Maisha na Karama za Ummul-Banin”, kimeandikwa na Ashraf Zahiri Ja‘fari, kikatarjumiwa na Husayn Mahfoudhi Musawi, Qum.

Kauli za Wanazuoni Kuhusu Ummul-Banin

Shahid Thani amesema kuhusu Ummul-Banin (a.s.): “Ummul-Banin alikuwa miongoni mwa wanawake wenye maarifa na fadhila nyingi. Alikuwa na mapenzi ya dhati na ya kina kwa familia ya Utume, na alijitolea kabisa katika kuihudumia. Familia ya Utume nayo ilimheshimu kwa daraja ya juu, na katika siku za Iddi walikuwa wanamtembelea kwa heshima.”

Sayyid Muhsin Amin katika kitabu A‘yan al-Shi‘a ameandika: “Ummul-Banin alikuwa mshairi mwenye ufasaha, kutoka katika familia ya asili na yenye ushujaa.”

Sayyid ‘Abdul-Razzaq Musawi Muqarram (aliyefariki 1391 H) amesema: “Ummul-Banin alikuwa miongoni mwa wanawake wenye fadhila. Aliitambua haki ya Ahlul-Bayt vizuri, na alikuwa mwaminifu katika mapenzi yake kwao. Naye pia alikuwa na nafasi ya juu na heshima kubwa miongoni mwao.”

Ayatullah Sayyid Mahmud Husayni Shahroudi (aliyefariki 1394 H) amesema: “Mimi katika matatizo yangu, mara mia nasoma salawat kwa ajili ya mama wa Hazrat Abul-Fadhl al-Abbas (a.s.), yaani Ummul-Banin (a.s.), na hutimiziwa haja yangu.”

Ali Muhammad Ali Dukhayli, mwandishi wa Kiarabu wa kizazi hiki, kuhusu bibi huyu amesema:
“Ukuu wa mwanamke huyu unaonekana pale habari ya kuuawa kishahidi wanawe inafikishwa kwake asiipatie uzito, bali huuliza kwanza kuhusu usalama wa Imam Husayn (a.s.); kana kwamba Imam Husayn ndiye mwanawe,  na sio wale…”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha