Alhamisi 18 Desemba 2025 - 20:40
Muqawama ni Njia ya Heshima na Hadhi kwa Umma wa Kiislamu / Viongozi wa Muqawama Wanaendeleza Njia ya Imam Khomeini (ra)

Hawza/ Hujjatul-Islam Sheikh Al-Baghdadi, huku akisisitiza nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono mataifa yaliyodhulumiwa na mhimili wa muqawama, alisema: Muqawama ni njia ya heshima na hadhi ya Umma wa Kiislamu, na viongozi wa muqawama wanaendeleza njia ya Imam Khomeini (ra) kwa kushikamana na misingi na imani.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Mashhad, Hujjatul-Islam Sheikh Hasan al-Baghdadi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuhuisha Turathi za Wanazuoni Lebanon, jioni ya Jumatano tarehe 17 December, katika mkutano wa kimataifa wenye anuani isemayo “Iran ya Kiislamu; Safu ya heshima ya Kiislamu katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni”, uliyofanyika kwa njia ya mtandao, alieleza vipengele vya kiakili na kimkakati vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono mapambano ya Kiislamu na mataifa yaliyodhulumiwa.

Akiashiria kuwa mkondo wa fikra na mwelekeo wa kimkakati wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni njia ya kipekee na adimu katika ulimwengu wa leo, alisema: Njia hii imejengwa juu ya kutetea haki, kusaidia maskini na waliodhulumiwa, na kulinda mataifa yaliyodhulumiwa duniani, na kwa busara na hekima imesimama imara dhidi ya mikondo ya utawala-dhalimu na miradi ya kulazimishwa.

Kwa mujibu wake, hii ndiyo njia ile ile iliyowekwa na Imam Khomeini (ra), iliyofanikiwa kuikusanya Umma wa Kiislamu chini ya mazungumzo ya pamoja.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuhuisha Turathi za Wanazuoni Lebanon, akirejelea fatwa ya kihistoria ya Imam Khomeini kuhusu Palestina, alisema: Fatwa hii ilitoa suala la Palestina kutoka kuwa mada ya kikanda na ya Kiarabu tu, na kuligeuza kuwa suala la Kiislamu na la kimataifa; kwa namna ambayo dhamiri ya Umma wa Kiislamu na watu huru wa dunia iliamshwa juu yake.

Hujjatul-Islam Sheikh al-Baghdadi, hiku akisisitiza kuwa; Palestina leo ni chaguo la makusudi la Waislamu wote na watu huru duniani, aliongeza kusema: Uamsho wa Kiislamu na mkondo wa maqawama ulipinga miradi ya mgawanyiko, udikteta na udhalilishaji wa mataifa iliyokuwa ikifuatwa chini ya mifumo ya bandia ya kikanda; katika muktadha huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, licha ya vikwazo, mashinikizo ya kisiasa na uadui unaoendelea, imegeuka kuwa nguzo kuu katika kuiunga mkono Palestina na kukabiliana na utawala wa Kizayuni.

Alitaja uongozi wa kidini na misingi halisi ya Uislamu kuwa ni kigezo cha njia hii, na kubainisha: Uislamu unaosisitizwa na Jamhuri ya Kiislamu haukubaliani na utawala, uvamizi na kugawanywa kwa mataifa. Kinachoshuhudiwa leo Afghanistan, Syria, Lebanon na maeneo mengine ni matokeo ya muqawama ya kihistoria kati ya uhuru na utawala; na muqawama katika njia hii haujajengwa juu ya kuomba huruma, bali juu ya imani na kusimama imara.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuhuisha Turathi za Wanazuoni Lebanon, akirejelea operesheni ya Tufan al-Aqsa, aliitaja kuwa ni nukta ya utofauti ya awamu mpya ya muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni, na kusema: Operesheni hii ilikuwa ni kilio kilichotokana na imani na uelewa, kilichogeuka kuwa mwitikio wa Umma wa Kiislamu, na ikaonesha kuwa mhimili wa mapambano ni mhimili wa nguvu halisi na una uwezo wa kubadilisha mizani ya vita; kinachotokea leo katika uwanja wa matukio ya kikanda ni matokeo ya moja kwa moja ya uthabiti wa Jamhuri ya Kiislamu na mataifa yenye imani katika kushikamana na misingi na itikadi zao.

Alisisitiza: Tufan al-Aqsa haikuwa hatua ya kihisia au upofu, bali kilikuwa kitendo cha uelewa, chenye malengo na kilichojengwa juu ya imani ya kina ya kidini, kilichovunja ukimya uliotawala duniani na kufichua sura halisi ya wanaodai haki za binadamu. Mwitikio wa viongozi wa Magharibi na uungaji wao mkono wa wazi kwa utawala wa Kizayuni pia ulionesha kuwa kigezo chao si haki, bali ni maslahi na nguvu.

Hujjatul-Islam Sheikh al-Baghdadi alielezea makabiliano haya kuwa ni mapambano ya Kiungu na akaongeza: Muqawama huu umeziunganisha Palestina, Lebanon, Yemen na nyanja zote za muqawama. Leo, haki ya muqawama imekuwa wazi zaidi kuliko wakati mwingine wowote, na batili—hata kama imejihami kwa silaha na vyombo vya habari—imehukumiwa kutoweka. Ahadi ya Mwenyezi Mungu haitenguki, na ushindi wa mwisho ni wa wale wanaosimama juu ya haki.

Katika kuendelea, alitaja kauli na misimamo ya viongozi wa muqawama, akiwemo Sayyid Hasan Nasrallah na Sheikh Na‘im Qasim, kuwa ni mwendelezo wa njia ya Imam Khomeini, na kusema: Njia hii ni njia ya heshima, uungwana na hadhi ya Umma wa Kiislamu; si njia ya kusalimu amri, bali ni njia ya subira, uelewa, busara na jihadi dhidi ya dhulma na uvamizi.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuhuisha Turathi za Wanazuoni Lebanon, mwishoni, alibainisha kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo, kwa ujasiri, hekima na kushikamana na misingi, inachora mustakabali tofauti katika eneo; mustakabali ambao ndani yake utawala wa Kizayuni utaanguka kama jengo dhaifu, na mataifa yaliyo shikamana na muwawama yatapata ushindi kwa mujibu wa ahadi ya Mwenyezi Mungu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha