Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Subhani katika kikao chake na wajumbe wa Baraza la Kielimu pamoja na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya I‘itikafu, huku akitoa pongezi kwa shughuli zilizofanyika katika kueneza ibada ya kiroho ya itikafu, alisisitiza juu ya nafasi ya msingi ya kiroho katika hakika ya uwepo wa mwanadamu.
Alieleza kuwa: sehemu muhimu ya ubinadamu wa mwanadamu inarejea kwenye maanawi, na endapo maanawi yataondolewa kwa mwanadamu, hakika ya ubinadamu wake utadhoofika. Kuelekea kwa Mwenyezi Mungu na kuzingatia ulimwengu wa juu ni sehemu ya maumbile na asili ya mwanadamu, na kudhani kuwa mapenzi ya Mungu ni jambo geni kwa utambulisho wa mwanadamu ni uelewa potofu wa hakika ya fitra (asili) ya Mwenyezi Mungu aliyomuumba mwanadamu.
Marji' huyu wa taqlidi, akirejea nafasi ya ibada za Kiislamu katika kumuongoza mwanadamu kuelekea kwenye maanawi, aliongeza kuwa: Miongoni mwa ibada muhimu zaidi zinazomwelekeza mwanadamu kwenye ulimwengu wa juu ni itikafu; ibada ambayo kwa kujitenga na shughuli za kila siku na mambo ya kimaada, mwanadamu hupata fursa ya kurejea kwa Mwenyezi Mungu, kwa fitra na ndani ya nafsi yake. Umuhimu wa itikafu ni mkubwa kiasi kwamba Mtume Mtukufu (s.a.ww), baada ya kushindwa kuitekeleza kutokana na Vita vya Uhud, mwaka uliofuata alikaa itikafu kwa siku ishirini, na katika riwaya nyengine muda tofauti wa itikafu yake umetajwa.
Ayatullah Subhani, akigusia hali ya ulimwengu wa leo na kutawala kwa mtazamo wa kimaada katika maisha ya wanadamu, alisisitiza kuwa: Kadiri tunavyoweza kwa mbinu sahihi, za busara na zilizo sawa kuwaelekeza watu kuelekea kwenye maanwi, matatizo mengi ya mtu binafsi na ya kijamii yatapata ufumbuzi, maisha yatakuwa matamu zaidi, na moto wa vita na ubinafsi utapungua.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akihimiza kukumbushwa baadhi ya hukumu za kisheria za itikafu, alisisitiza juu ya ulazima wa kuzingatia uharamu wa biashara katika siku za itikafu, na akabainisha kuwa: katika miji kama Qum, maandalizi yanayohitajika kwa wakaaji itikafu yapo, lakini katika maeneo yenye idadi ndogo ya watu, uangalizi mkubwa zaidi unahitajika katika kuzingatia hukumu za kisheria.
Mtukufu huyo pia alisisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha maudhui ya kiroho ya itikafu, akasema: inapasa katika kila mchana na usiku angalau wahubiri wawili—mmoja asubuhi na mwingine alasiri au usiku—wajikite kwa umakini katika kuelezea masuala ya kiroho na kimaadili; kwa kuwa maanwi ndio msingi wa utambulisho wa mwanadamu, na kujitenga na hilo husababisha kudhoofika kwa ubinadamu.
Ayatullah Subhani, akiendelea kugusia hali ya ulimwengu wa Kiislamu, aliwaomba wakaaji itikafu katika siku za itikafu waombe dua kwa ajili ya kuwaokoa Waislamu kutoka katika hali ngumu ya sasa, kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu na kuondolewa kwa dhulma. Aliongeza kuwa: mambo yanayowakumba Waislamu leo hayana mfano wa karibu katika historia, na kutojali kwa dunia kuhusu maafa haya kunazidisha wajibu wa dua, tawasuli na uamsho wa Umma wa Kiislamu.
Mwisho, kwa kusisitiza umuhimu wa dua na tawasuli mbele ya njama za maadui wa Uislamu, aliwatakia mafanikio wahusika wa itikafu na akaeleza matumaini kuwa harakati hii ya kiroho itakuwa chachu ya kuimarika kwa imani, maadili na umoja katika jamii ya Kiislamu.
Maoni yako