Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, wakati mvutano wa Mashariki ya Kati ukiendelea kuongezeka, serikali ya Venezuela kwa sauti isiyo ya kawaida imekemea vikali mashambulizi yanayofanywa na Israel dhidi ya Palestina, Lebanon na Syria na ikakosoa vikali ukimya wa taasisi za kimataifa mbele ya “mchakato unaoelekea kwenye janga la mauaji ya raia.” Caracas imesisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa lazima iingilie kati kabla ya mgogoro kupata sura mpya.
Serikali ya Venezuela kwa kutoa taarifa kali, mara nyingine tena imekemea mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina, Syria na Lebanon na kuyaita “uhalifu wenye ukatili usioweza kufikirika”; uhalifu ambao kwa mujibu wa maafisa wa Caracas, si kwamba unapungua bali kila siku unaongezeka zaidi.
Yvan Gil, waziri wa mambo ya nje wa Venezuela, katika ujumbe wake kwenye jukwaa la Telegram, alichora taswira ya kutisha ya hali ya eneo na kuandika: “Mabomu ya mara kwa mara, mauaji ya watu wasio na ulinzi na uharibifu kamili wa vijiji na vitongoji, vimekuwa jambo la kawaida kwa utawala unaojihusisha kwa kinga kamili.” Alisisitiza kwamba Israel, chini ya ukimya wa nguvu za dunia, imegeuka kuwa mchezaji anayejiweka juu ya kanuni na sheria zote.
Gil akirejelea jukumu la Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alimwona kama mwenye jukumu la kutekeleza sera ambazo ni “mfano wa wazi wa ukatili na uhalifu dhidi ya ubinadamu.” Takwimu zilizotolewa na maafisa wa Venezuela zinaonesha kwamba tangia kuanza kwa mashambulizi makubwa Oktoba 2023 hadi sasa, karibu Wapalestina 70,000 wameuawa na zaidi ya 171,000 kujeruhiwa; idadi ambayo kwa mujibu wa wachambuzi ni “isiyo na mfano katika historia ya kisasa ya eneo.”
Waziri wa mambo ya nje wa Venezuela pia alikosoa kile alichokiita “kupooza kwa taasisi za kimataifa.” Alisema: Mahakama ya Kimataifa ya Haki, hadi sasa haijafanikiwa hata kuchukua msimamo wazi na wenye ufanisi mbele ya kiwango hiki cha mauaji. Ikiwa jumuiya ya kimataifa katika hali kama hii haiwezi kuchukua hatua, basi kuwepo kwa taasisi hizi kuna maana gani?
Caracas iliendelea kutangaza kwamba; itaendeleza msaada wake kwa mataifa ya Syria, Palestina na Lebanon na mara nyingine tena ikaiomba jumuiya ya kimataifa kuchukua “hatua za haraka, za vitendo na zisizo na hiyana” ili kuzuia kuongezeka zaidi mgogoro. Venezuela imesisitiza kwamba ukimya wa kimataifa si kwamba unasaidia kutatua mgogoro, bali unaufanya kuwa mrefu na wa uharibifu zaidi.
Katika sehemu nyingine ya ripoti imesema kwamba; licha ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kusitisha vita, makubaliano haya kimsingi yamekuwa hayana athari. Israel inasema Wapalestina hawazingatii ahadi zao na kwa sababu hiyo mashambulizi yanaendelea; ilhali nchi wakosoaji wanasema dai hili ni kisingizio cha kuendeleza operesheni za kijeshi.
Yvan Gil mwishoni, mara nyingine akiihutubia jumuiya ya kimataifa alionya kwa kusema: Imetosha. Dunia haiwezi kuendelea kupita pembeni ya janga hili, wakati wa uwajibikaji umefika; lazima kwa sauti kubwa isemwe: "Vita vikome", "Mauwaji yakome", "Wahalifu waondoshewe kinga".
Maoni yako