Jumatano 17 Desemba 2025 - 17:00
Muqawama ni Jibu la Kihistoria kwa Uislamu Dhidi ya Uvamizi na Ubeberu

Hawza/ Hujjatul-Islam Sheikh Baghdadi, huku akisisitiza kuwa; muqawama una mizizi yake katika mafundisho halisi ya Uislamu, alisema wazi kuwa: Muqawama ni jibu la kihistoria na la kimkakati la Uislamu dhidi ya uvamizi, ubeberu na tamaa ya kutawala. Katika historia yote, muqawama umejitokeza kulingana na mazingira katika sura za kijeshi, kisiasa, kitamaduni na kijamii, na umefanikiwa kumzuia adui kufikia malengo yake.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Mashhad, Hujjatul-Islam Sheikh Hassan al-Baghdadi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kufufua Turathi za Wanazuoni wa Lebanon, katika kongamano la kwanza la kimataifa la “Teolojia ya Muqawama” lililofanyika leo Jumatano tarehe 17 December katika Kitivo cha Sayansi cha Chuo Kikuu cha Ferdowsi cha Mashhad Iran, alifafanua nyanja mbalimbali za dhana ya muqawama na kusisitiza umuhimu wa kuuelewa mkakati huu kwa undani na kwa tabaka nyingi katika hali ya sasa ya eneo.

Alitoa shukrani zake kwa rais wa chuo kikuu, wajumbe wa baraza la uongozi, wakuu wa vitivo na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Ferdowsi Mashhad kwa juhudi na shughuli zao za kielimu katika kuandaa kongamano hili muhimu katika mazingira nyeti ya sasa.

Mjumbe wa Baraza la Wanazuoni wa Lebanon aliendelea kuwasilisha salamu na pongezi za Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, kwa wahudhuriaji na akasema: “Kwa niaba yake nimepewa jukumu la kuhudhuria kongamano hili lenye thamani; kwa kuwa tukio hili la kielimu katika kipindi hiki nyeti na katika mazingira maalumu yanayolikabili eneo letu lina umuhimu wa kimkakati.”

Hujjatul-Islam Sheikh al-Baghdadi, akirejea mabadiliko ya kikanda, alisema: leo eneo letu linakabiliwa na sera za kiburi na ukatili za Marekani na washirika wake, hususan Wazayuni; sera ambazo lengo lake ni kuzikalia ardhi, kutawala rasilimali na mali, kuyafunga mataifa, na kupambana na Uislamu mtukufu.

Aliendelea kufafanua dhana ya muqawama akasema: inapozungumziwa kuhusu muqawama, mara nyingi hujitokeza dhana kwamba muqawama una maana tu mbele ya ukaliaji; ilhali uhalisia ni kwamba muqawama, kulingana na mazingira na mahitaji, una aina nyingi — kuanzia muqawama wa kijeshi na kisiasa hadi muqawama wa kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kufufua Turathi za Wanazuoni wa Lebanon aliongeza kuwa: katika baadhi ya nyakati, muqawama hujitokeza katika sura ya subira, kusimama imara na kumzuia adui kufikia malengo yake; kama ilivyokuwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.ww) katika kipindi cha kuwepo Makka kabla ya kuhama kwenda Madina.

Alisema pia: katika nyakati nyingine, muqawama huchukua sura ya hatua ya moja kwa moja na ya kushambulia; kama ilivyotokea katika Vita vya Badr Kubwa, baada ya idhini ya Mwenyezi Mungu, hatua hiyo ilianza. Na katika hatua nyingine, muqawama hujitokeza kwa sura ya kujilinda na kustahimili; kama ilivyotokea katika Ghazwa ya Ahzab na Vita vya Handaki.

Akirejea ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa wapiganaji katika njia ya haki, Hujjatul-Islam Sheikh al-Baghdadi alisisitiza: pale Waislamu wanapobaki imara, kama walivyosimama imara katika Vita vya Ahzab, na kama tunavyoshuhudia leo katika vita vilivyolazimishwa kuanzia Palestina, Lebanon na Yemen hadi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, basi ahadi ya Mwenyezi Mungu hutimia; pale anaposema: “Na Mwenyezi Mungu aliwarithisha ardhi zao, nyumba zao na mali zao, na ardhi ambayo hamjawahi kukanyaga; na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.”

Hujjatul-Islam Sheikh al-Baghdadi, akigusia maendeleo ya hivi karibuni ya kivita, alisema: uthabiti na subira kubwa ya mataifa, hususan nchini Lebanon katika kipindi cha siku sitini na sita za muqawama, ulipelekea adui kushindwa kuingia vijijini, na zaidi ya maafisa na wanajeshi sabini na tano wa Israel, licha ya uungwaji mkono kamili wa Marekani, walishindwa na kulazimika kurudi nyuma.

Aliongeza kuwa: kufuatia uvamizi dhidi ya Yemen na mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tulimpiga adui mapigo mazito; kuanzia Tel Aviv hadi Be’er Sheva na maeneo mengine, hadi pale wao wenyewe walipoomba kusitishwa kwa mapigano mara moja, kwa haraka na bila masharti yoyote.

Mwisho, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kufufua Turathi za Wanazuoni wa Lebanon aliibua maswali ya kutafakari akasema: mara nyingi tumeeleza kuhusu hasara zetu; Katibu Mkuu wa Hizbullah na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu wameligusia suala hili. Lakini je, maadui wana ujasiri wa kuzungumzia hasara kubwa walizopata kutoka katika mikono ya muqawama wa Palestina, Lebanon, Yemen, na hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran? Je, wana cha kusema kuhusu kufilisika na kuondoka kwa makampuni makubwa, na kuongezeka kwa chuki ya kimataifa dhidi ya Marekani na Israel? Kama wanaweza, basi waache wazungumze.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha